ASSAs

TCAA YAWATAKA FASTJET KUPELEKA ANDIKO

829
0
Share:

Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA ), imelitaka Shirika la Ndege la Fastjet Tanzania kupeleka andiko la kudhibitisha uwezo wa kifedha ili kuona kama wanajiweza katika biashara hiyo ya usafishaji wa anga.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Desemba 27, 2018 mkurugenzi mkuu wa TCAA, Hamza Johari amesema shirika hilo lina madeni zaidi ya bilioni 6 hivyo kwa mujibu wa sheria  ni lazima madeni yote yalipwe ili kuendelea na biashara hiyo.

“Madeni ya Fastjet yalikuwa zaidi ya Sh6 bilioni ambazo wanadaiwa na watu tofauti, tayari wamelipa sehemu ya fedha wanazodaiwa na TCAA japo si zote. Usafiri wa ndege una masharti ya msingi ambayo yasipofuatwa ni hatari,” amesema Johari.

Akifafanua baadhi ya masharti ya usafiri wa anga amesema ni pamoja na “uwezo wa kifedha katika shirika, usafiri wa anga hakuna ujanja kama hatakidhi masharti leseni itafutwa tukisema tuhurumiane ni hatari tutaua watu, usafiri wa anga usiposimamiwa vizuri ni hatari kwa usalama utaua watu.”

Hamza amesema kwamba tangu shirika hilo lipewe notisi ya kusudio la kufutiwa leseni Desemba 17, 2018, liliwasilisha andiko lake Desemba 24, 2018 na sasa bado mamlaka hiyo inalifanyia kazi.

Aidha mamlaka hiyo imesema kwamba ndege aina ya Embraer 190 iliyokodiwa baada ya Fastjet kufungiwa haitaruhusiwa kuondoka nchini mpaka Fastjet walipe madeni wanayodaiwa.

Ameongeza kwamba, “FastJet itakufa kwasababu zao wenyewe maana wanamatatizo mengi, TCAA tunasimamia sheria ili kulinda usalama wa abiria, kulinda maslahi ya watoa huduma (supplies). Habari zote zilizoelezwa si za kweli ni upotishaji mtupu.”

Pamoja na hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo Lawrence Masha alinukuliwa akisema “TCAA inasema ili niweze kuingiza ndege, nimalize kwanza madeni yote, baadhi ya madeni tayari yamelipwa na Fastjet Plc mengine Fastjet Tanzania tumemaliza lakini fedha imeisha, kwa kuwa tayari fedha nyingine tulizitumia kutimiza matakwa yao, wangeniruhusu nifanye kazi ili nipate fedha ya kulipa yaliyobaki.”

(Visited 59 times, 1 visits today)
Share this post