ASSAs

KIJANA INITIATIVE FOUNDATION YALETA NEEMA MOROGORO

771
0
Share:

Taasisi ya Kijana Initiative Foundation imeungana na familia (100) zinazoishi katika mazingira magumu wakiwemo wajane pamoja na wanawake wajasiriamali wadogo kubadilishana mawazo na kula chakula cha pamoja katika ukumbi wa Chuo Kikuu Cha Jordan mkoani Morogoro.

Katika hafla hiyo iliyojumuisha viongozi mbalimbali akiwemo,  Ndg Shaka Hamdu Shaka Katibu wa CCM Mkoa wa Morogoro, wanawake wajasiriamali pamoja na familia zinazoishi katika mazingira magumu zimeonesha furaha ya wazi kwa msaada mkubwa wanaoupata.

Aidha, Shaka amesisitiza  kuwa kama CCM mkoa wa Morogoro watahakikisha wanawake hao wajasiriamali wanapata mitaji zaidi ili kuondokana na utegemezi kama ilivyokuwa sasa.

“Hii taasisi ya Kijana Initiative foundation inafanya kazi nzuri sana, mimi ninawaunga mkono na wakati wote waje ofisini kwangu nitawasaidia kwa kadri itakavyowezekana kwa sababu haya yote wanafanya wanatekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, tunahitaji Taasisi kama hizi zinazogusa maisha ya watu na tutahakikisha wanawake hawa wanapata mikopo”. Shaka amesisitiza.

Naye,  Said Said Nguya, amesema, “Hawa ni wananchi wanyonge, na Rais Magufuli hawa ndio watu ambao kila siku anawatetea ili wajikwamue kutoka hapa walipo, naomba muendelee kuwasaidia zaidi na zaidi ili watoto hawa katika familia hizi waje kuwa tegemeo kwa Taifa letu, pale mnapokwama ama kukwamishwa na mtu yeyote kwa matakwa yake, kimbilio lenu ni Chama Cha Mapinduzi.”

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Grace Meena kwa kushirikiana na Mgeni Rasmi wamegawa Vifaa mbalimbali vya shule ikiwemo Madaftari, kalamu, na sare kwa watoto kutoka familia hizo na kuweka bayana mpango wao wa kuwatafutia mitaji familia hizi ili zijikwamue katika hali walionayo sasa.

Wageni wengine waliohudhuria katika hafla hiyo ni pamoja na Katibu wa Vijana Mkoa wa Morogoro Ndg Isack Kalaiya na Muwakilishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya. Ambapo wote kwa pamoja wameonesha kuguswa na changamoto za familia hizi na kuahidi kutoa ushirikiano wa usaidizi ili zijikwamue kutoka hapa zilipo .

(Visited 72 times, 1 visits today)
Share this post