ASSAs

ASKARI ALIYEPATA CHEO ALINUSURIKA KUUAWA NA MAJAMBAZI

2308
0
Share:

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Jonathan Shanna akimvisha cheo Konstebo WP. 12415 Dominica Michael Nnko cheo kuwa Koplo kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Simon Sirro baada ya kujwatunukia vyeo hivyo.

…………………………….

NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA

MMOJA wa askari watano waliotunukiwa vyeo na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Simon Sirro, kutokana na utendaji wao amesema kuwa alinusurika kupigwa risasi na jambazi wakati wakijiandaa kuwakabili katika eneo la Nyegezi,jijini Mwanza.

Askari huyo WP 12415 Dominica Michael ambaye ametunukiwa cheo cha Koplo amesema wakati akizungumza na mtandao huu muda mfupi baada ya kuvishwa cheo hicho na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza Jonathan Shanna kwa niaba ya IGP Sirro.

Alisema kuwa   Februari 2017,  alinususurika kuuawa kwa kupigwa risasi baada ya kuwahiwa na jambazi lakini kwa ujasiri alitumia mbinu ya uaskari kuwahi kulala chini kabla jambazi huyo kufariki kwa kupigwa risasi na askari wenzake.

Koplo Michael alieleza kuwa usiku wa siku ya tukio hilo laambayo ilikuwa  siku ya kuzaliwa kwake, walipangwa kuwakabili majambazi huko Nyegezi, kumbe eneo walikopangwa aliwahiwa na jambazi mmoja bila kumuona ambaye alimlenga kwa bunduki .

  “Kwanza nashukuru kwa kupata cheo hiki ambacho sikukitarajia ambacho kinatokana na viongozi kutambua mchango wangu katika kulinda usalama wa raia na mali zao.Maishani mwangu sitasahau tukio la Februari 19, 2017 ambayo ilikuwa siku ya kuzaliwa kwangu nilinusurika kuuawa nikiwa kazini,” alisema Koplo Michael na kuongeza;

“Tukiwa katika mapambano na majambazi nilipagwa kwenye eneo tulikokuwa mmoja wa majambazi aliniwahi akitaka kunipa kwa risasi, kwa ujasiri, ukakamavu na mbinu za uaskari niliwahi kulala chini hivyo akanikosa kabla ya kuuawa na askari wenzangu.” 

Alidai kuwa licha ya changamoto ya kufanya kazi ya kupambana na wahalifu katika miundombnu isiyo rafiki cheo hicho kimemuongezea, ujasiri, ukakamavu na kujituma kwa bidii kwenye utendaji wake na ushirikiano na wenzake.

Askari mwingine  ambaye alishiriki kuokoa majeruhi wa ajali ya kuzama kwa kivuko cha MV. Nyerere Amon John alitunukiwa cheo cha Meja kutoka Sajenti Meja na kusema kuwa kwenye ajali hiyo alifanya kazi ya uokoaji kwa siku tatu bila kula usiku na mchana.

 Aidha, Mrakibu Msaidizi wa Polisi Levina Jeremiah ambaye naye alipandishwa cheo na Rais John Magufuli  kutoka Mkaguzi Msaidizi alisema atakitendea haki cheo hicho ili kumwonyesha Rais na viongozi wake kuwa hawakukosea.

Askari huyo ambaye alikuwa masomoni kwenye mafunzo ya uongozi jijini Dar es Salaam alikuwa miongoni mwa askari maofisa 10 bora kati ya 515 na kutunukiwa cheti cha heshima kutokana na kufanya vizuri kwenye masomo ya darasani,nje na nidhamu.

Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongela amewakabidhi vyeti na kuwazawadia askari waliopata vyeo sh.200,000 kila mmoja na ofisa mmoja sh. 300,000 kutokana na utendaji wao wa weledi uliouletea sifa mkoa huo.

Akizungumza na maaskari baada ya kuwakabidhi vyeti Ofisa mmoja wa polisi na askari wengine watano Mongela alisema wananchi wanafanya shughuli za maendeleo kutokana na usalama wa uliopo mkoani humu kwa sababu askari polisi wanafanya kazi kwa weledi.

Alisema weledi huo umedhihirika baada ya askari waliokuwa mafunzoni kuwa miongoni mwa askari weledi lakini pia waliotimiza majukkumu yao kwa kupambana na kufanikiwa kuwauwa majambazi saba na kuokoa silaha sita kutoka mikononi mwa majambazi hao.

“Kama ilivyo kauli mbiu yenu ya Tenda kwa Weledi hakuna bla blaa Hapa Kazi Tu! Mwanza hakuna unyanyasaji na uonevu, kazi zinafanyika na najivunia sana utendaji wenye weledi unaofanywa na polisi na mkoa unabebwa na sifa hiyo,”alisema Mongela.

Alieleza kuwa wakati mwaka unaelekea mwishoni Mwanza ilikuwa salama licha ya matukio kadhaa yaliyotaka kuchafua taswira yake lakini kwa weledi wa hali ya juu yalidhibitiwa na hivyo anaamini wananchi watasherehekea salama mwaka mpya kwa amani na utulivu.

Hata hivyo alionya watu wenye tabia ya uhalifu wanaodhani kuwa muda wa kusherehekea mwaka mpya ndio muda wa kutimiza malengo yao wasithubutu kwani watadhibitiwa na watakaojaribu wasije kulaumu baadaye.

Pia aliwataka wananchi kuwa wazalendo na walinzi wa maeneo yao kwa kuwa ndio walinzi wa kwanza na kuahidi kuwapa zawadi ya fedha askari walipata vyeo mbali na zawadi y ash. 200,000 na 500, 000 walizopewa awali.

(Visited 385 times, 1 visits today)
Share this post

Contact Us