ASSAs

SIMBA SC WAITANDIKA CHIPUKIZI KOMBE LA MAPINDUZI CUP BAO 4-1

1805
0
Share:

SIMBA SC imeanza vyema michuano ya Kombe la Mapinduzi baada ya ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Chipukizi ya Pemba Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Nyota wa mchezo wa leo alikuwa ni mshambuliaji wake wa kimataifa wa Rwanda mwenye asili ya Uganda, Meddie Kagere aliyefunga mabao mawili kwenye ushindi huo.
Kagere aliye katika msimu wake wa kwanza tu Simba SC, alifunga mabao yake katika dakika za 33 na 59, wakati mabao mengine ya Wekundu hao wa Msimbazi yamefungwa na beki Mghana, Nicholas Gyan dakika ya 56 na Nahodha, John Raphael Bocco kwa penalti dakika ya 83.
Bao pekee la Chipukizi katika mchezo wa leo limefungwa na mchezaji wake nyota, Evidence Godwin Kilongozi dakika ya 55.

Baada ya mchezo wa leo, Simba SC watarejea uwanjani Jumapili kumenyana na KMKM na kumalizia na Mlandege Januari 8, mechi zote zikanzia Saa 2:15 usiku.
Baada ya hapo, kikosi cha Simba SC kitasafiri kurejea Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo wake wa kwanza wa Kundi D Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya JS Saoura ya Algeria Januari 12 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
Na kama timu itafuzu Nusu Fainali, nyota wachache ambao hawatakuwamo kwenye programu ya mechi dhidi ya JS Saoura wataongezewa na wachezaji wa timu ya vijana kucheza hatua hiyo na timu ikifanikiwa kuingia fainali, kikosi kizima kitarejea kumalizia mashindano. 
Kikosi cha Chipukizi kilikuwa; Yussuf Abdu Ali, Juma Kassim Seif, Kheri Fadhil Kassim, Khamis Mohamed Hassan, Samir Said Sanze, Said Khamis Omar, Evidence Godwin Kilongozi/Abdallah Mohamed Masoud, Shaaban Iddi Mtongole, Ibrahim Kombo Ali/Omar Juma Haji, Twalib Khamis Abeid na Mundhir Iman Mohamed/Rashid Said Salum.
Simba SC; Ally Salim, Nicholas Gyan/Zana Coulibaly, Asante Kwasi, Yusuph Mlipili, Paul Bukaba, Muzamil Yassin, Haruna Niyonzima, Said Ndemla, Adam Salamba/Rashid juma, Meddie Kagere/John Bocco na Hassan Dilunga/Mohammed ‘Mo’ Ibrahim.

(Visited 125 times, 1 visits today)
Share this post

Contact Us