ASSAsSamaki Samaki

MGOMBEA ALIYESHINDWA UCHAGUZI WA URAIS ATAKA KUPINGA MATOKEO MAHAKAMANI

199
0
Share:

Mgombea wa upinzani aliyeshindwa katika uchaguzi wa Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) uliofanyika Disemba 30 ameapa kuyapinga matokeo mahakamani.

Martin Fayulu ameiambia BBC kuwa raia wa Congo wanastahili kujua ukweli wa uchaguzi, mabao ameutaja kuwa ni “mapinduzi”.

Mgombea mwengine wa upinzani Felix Tshisekedi, alitangazwa kuibuka na ushindi katika kinyang’anyiro hicho, lakini kumekuwa na tuhuma kuwa mshindi huyo ameingia makubaliano ya kisiasa na rais aondokaye Joseph Kabila.

Tayari watu kadha wanaripotiwa kuuawa na wengine kujeruhiwa toka matokeo hayo yalipotangazwa.

Uchaguzi huo unakamilisha safari ya miaka 18 madarakani ya Joseph Kabila.

Matokeo hayo, endapo yatathibitishwa, yataweka historia ya makabidhiano ya amani ya hatamu za uongozi toka nchi hiyo ilipopata uhuru wake toka kwa wakoloni wa Ubelgiji mwaka 1960.

Kanisa lenye ushawishi mkubwa la Katoliki ambalo lilikuwa na waangalizi wa uchaguzi 40,000 limesema matokeo yaliyotangazwa hayaendani na matokeo waliyonayo.

Fayulu amesema nini?

Akiongea na mhariri wa BBC wa Afrika Fergal Keane, Bw Fayulu amesema atayapinga matokeo hayo kwenye mahakama ya katiba.

Haki miliki ya pichaAFP
Image caption
Maswali yanaulizwa iwapo Kabila ametia mkono wake kwenye matokeo yaliyotangazwa
“Nitafanya kila liwezekanalo kwangu kufanya ukweli udhihiri sababu Wacongo wanataka mabadiliko,” amesema.

Fayulu hata hivyo ameweka wazi kuwa kuna uwezekano mdogo wa kushinda kesi hiyo sababu mahakama “imeundwa na watu wa Kabila” lakini amesema hataki kuwapa kisingizio wapinzani wake kuwa hakufuata sheria.

“Felix Tshisekedi ameteuliwa na Kabila ili kutekeleza matakwa ya utawala wa Kabila. Kabila ndiye bosi,” amedai Fayulu.

“Kabila hawezi kubaki na kusuka mpango na mtu ambaye hatakuwa na mamlaka yeyote… Tshisekedi anajijua kwamba hakushinda uchaguzi.”

Fayulu amesema ana hofu kuwa kutatokea vurumai kama tume ya uchaguzi (Ceni) haitatoa takwimu sahihi za “kituo kimoja kimoja cha kupigia kura” na kusisitiza kuwa ni haki ya kila Mkongomani kuandamana kwa mujibu wa sheria.

Maelfu ya mashabiki wa Tshisekedi wameingia mitaani kwa furaha kusherehekea ushindi walioupata, lakini upande wa pili wafuasi wa Fayulu wamejitokeza mitaani kupinga matokeo hayo.

Matukio ya ghasia yameripotiwa katika eneo la Kikwit, ambapo polisi wawili na raia wawili wanasemakana kuuawa.

Kuna ripoti pia mamia ya wanafunzi wamekuwa wakipinga matokeo hayo kwa kuandamana na kutimuliwa na mabomu ya machozi katika mji wa Mbandaka.

Maandamano pia yameripotiwa katika eneo la Kisangani, lakini kusini ambapo Tshisekedi anaungwa mkono kwa wingi kumekuwa na sherehe.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Antonio Guterres amezitaka pande zote kujizuia kufanya ghasia.

(Visited 14 times, 1 visits today)
Share this post