ASSAs

FATMA KARUME AKANUSHA KUJIHUSISHA NA CHAMA CHOCHOTE CHA SIASA

1917
0
Share:

Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika, Fatma Karume amekanusha kuwa mwanachama wa Chama chochote cha siasa nchini  na kwamba wananchi wasipotoshwe kwa namna yoyote ile.

Bi. Karume ameyasema hayo alipokuwa akikosoa andiko lililochapishwa kwenye ukurasa wa Facebook wa kada maarufu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Bw. Yericko Nyerere kwa madai kuwa mwanaharakati huyo ni mwanachama wa CCM tangu kuzaliwa.

Katika andiko alilolichapisha  Januari 13, Yericko alifafanua kuhusu Bi. Karume kukutana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamisi Kigwangalla na kueleza kwamba Fatma ana haki kwa kuwa siyo mwanachama wa chama chochote cha upinzani hivyo asiingiliwe, au kupangiwa namna ya kuishi .

“Fatma si mwanachama wa Chadema au chama chochote cha upinzani, ninachofahamu yeye ni mwanaccm tangu anazaliwa hadi leo. Sasa akiwa kama Mwanaharakati, akikutana na wananchi wenzake kosa liko wapi?. Akiwa kama mwanaccm, akikutana na wanachama wenzake kosa liko wapi?, akiwa Rais wa TLS, akikutana na wadau kosa liko wapi?”, amehoji Nyerere Fatma Karume akiwa pamoja na Waziri Hamisi Kigwangalla.

Hata hivyo baada ya andiko hilo Bi. Karume ameeleza kuwa hataki kuendeshwa na Itikadi za siasa na kwamba anapenda uhuru wake.

“Yericko Nyerere, CCM Tanzania ninataka kukuelezeni mimi sio mwanachama wa chama cha siasa chochote!. Naomba tuheshimiane kwa hilo. Acheni kupotosha wananchi, ninapenda uhuru wangu, sitaki kuendeshwa kwa itikadi za siasa zozote. Napiga kura ninavyojisikia mimi,” – Bi. Karume.

Hata hivyo kwa kuonyesha uungwana kada huyo amemshukuru Bi. Karume kwa kutoa ufafanuzi wazi jambo ambalo litaondoa mkanganyiko.

“Asante sana shangazi kwa kufafanua wazi hili, tulikuwa katika mkanganyiko uliozusha mjadala huku mitandaoni, kwa niaba ya wengine nikuombe radhi kwakukubatiza itikadi ya kisiasa isiyo sahihi,” amesema Nyerere.

(Visited 236 times, 1 visits today)
Share this post

Contact Us