ASSAs

WAZIRI UMMY : UKOMA BADO NI TATIZO TANZANIA

1257
0
Share:

Dar es Salaam

Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema kuwa, ugonjwa wa ukoma bado ni tatizo kubwa nchini Tanzania licha ya juhudi mbalimbali zinazofanywa na mashirika ya ndani na nje ya nchi kuhamasisha na kutoa elimu kuhusu ugonjwa huo.

Kauli hiyo ameitoa mara baada kufanya ziara ya kutembelea makazi ya wazee Nunge, kigamboni jijini Dar es Salaam, jana ambapo amesema kwa mujibu wa Takwimu za 2017, jumla ya wagonjwa wapya 1,933 waligundulika kuwa na ukoma na hivyo kufanya kiwango cha ukoma kuwa watu 4 kwa kila watu 100,000.

“Jana nilitembelea makazi ya Wazee Nunge, Kigamboni nimepeana mikono na waathirika wa Ukoma ikiwa ni ishara ya kutekeleza kwa vitendo kauli mbiu yetu ya maadhimisho ya Siku ya Ukoma 2019 ya “Tutokomeze Ubaguzi, Unyanyapaa na Chuki dhidi ya Waathirika wa Ukoma”amesema Waziri Ummy.

Amesema kuwa,Takwimu hizo zinaifanya Tanzania kuendelea kuwa miongoni mwa nchi 22 zenye wagonjwa wengi wa ukoma duniani, nchi nyingine ni India, Indonesia, Brazil, Ethiopia, Msumbiji, Nigeria na DRC Congo.

Aidha amesema kuwa, kuna mikoa 10 ambayo hugundua wagonjwa wapya wengi zaidi,Mikoa hii ni Lindi, Mtwara, Pwani, Morogoro, Tanga, Dodoma, Geita, Kigoma, Rukwa na Tabora ambapo Wilaya 20 zenye kiwango kikubwa cha wagonjwa wapya wa Ukoma ni Liwale, Lindi Vijijini, Nachingwea, Ruangwa, Nanyumbu, Masasi Mjini, Pangani, Mkinga, Korogwe, Mvomero, Kilombero, Morogoro Vijijini, Ulanga, Shinyanga Manispaa, Chato, Mafia, Rufiji, Kilwa, Nkasi na Mpanda.

Ameongeza kuwa, Serikali kwa kushirikiana na wadau wataendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha ukoma unatokomezwa nchini, hivyo nitoe wito kwa jamii, wazazi na walezi kujenga tabia ya kuchunguza miili yetu na ya watoto wetu, endapo utaona mojawapo ya dalili za ukoma ni muhimu kwenda kituo cha Tiba kwa uchunguzi bila kuchelewa.

Waziri Ummy amezitaja dalili za Ukoma ni baka au mabaka mwilini yenye rangi ya shaba na hayana hisia, vijinundu kwenye ngozi au mishipa ya fahamu kuvimba, ganzi kwenye mikono au miguu, ambapo ugonjwa huo unatibika.

Hata hivyo, amesema ngonjwa aliyeanza tiba hawezi kuambukiza mtu mwingine hivyo hakuna sababu ya kumtenga, tiba ya Ukoma inapatikana nchini kote na hutolewa bila malipo kwa wagonjwa wote.

Aidha ameitaka jamii kuachana na imani potofu kuwa ukoma ni ugonjwa wa kurithi au kulongwa, Ukoma ni ugonjwa wa kuambukiza unaosababishwa na vimelea vinavyoshambulia mishipa ya fahamu na huambukizwa kwa njia ya hewa pekee.

Amesema kuwa, kutokana na ugonjwa huo kuwa unatibika ni vyema wagonjwa wa ukoma kuacha kuchelewa kujitokeza kupata matibabu hadi wanapopata ulemavu, ambapk amesisitiza pale mtu anapoona mabadiliko yoyote yanajitokeza kwenye miili yetu twende mapema ktk vituo vya Tiba kuchunguzwa ili tupate matibabu.

(Visited 82 times, 1 visits today)
Share this post