ASSAs

WAZIRI BITEKO AWATOA HOFU WAWEKEZAJI KUWEKEZA NCHINI

946
0
Share:

Waziri wa Madini, Doto Biteko amewatoa hofu Wawekezaji wa nje na kueleza kuwa, Mabadiliko yaliyofanywa katika Sheria ya Madini ya Mwaka 2017, hayana lengo la kuwakandamiza isipokuwa yamelenga katika kuifanya rasilimali madini kuwanufaisha wote, wawekezaji na watanzania.

Aliyasema hayo Januari 4, 2019 katika kikao baina yake na Balozi wa Canada nchini Pamela ODonnel, ambacho pia kilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, Kamishna wa Madini, Mhandisi David Mulabwa, Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango, Augustine Ollal.

Akielezea lengo la kuonana na uongozi wa juu wa Wizara, Balozi ODonnel alisema amefika ili kupata uelewa wa mabadiliko mbalimbali yaliyotokea katika sekta ya madini pamoja na maeneo mengine ili kuwatoa hofu wawekezaji kutoka katika taifa lake wanaopenda kuwekeza nchini.

Pamoja na nia yake ya kupata ufumbuzi kwa masuala ya Sheria ya Madini, Balozi ODonnel alihoji kuhusu masuala mengine ikiwemo utawala wa kisheria, mikataba ya madini, kodi na tozo mbalimbali pamoja na upatikanaji wa vibali vya kufanya kazi nchini kwa wananchi kutoka nchini Canada.

Akijibu hoja hizo, Waziri Biteko aliwataka wawekezaji kutoka nchini Canada kutokuwa na wasiwasi kwa mabadiliko hayo na kuwataka kutembelea ofisi ya madini ili kupata ufafanuzi wa jambo lolote lenye utata katika kufanikisha nia njema ya kuwekeza nchini. Tupo kwa ajili yao, wasisite kupata ufafanuzi wa jambo lolote linalohusu sekta ya madini,” alisisitiza.

Aliongeza kuwa, mataifa mbalimbali duniani yanafanya mabadiliko katika masuala mbalimbali na kueleza kuwa, si vibaya kwa Tanzania kufanya mabadiliko kwa jambo lolote ambalo lina manufaa kwa taifa.Madini ni rasilimali inayokwisha, hivyo ni muhimu madini yanapochimbwa yawaletee faida watanzania na pindi yatakapokwisha wajivunie rasilimali madini iliyokuwepo kutokana na maendeleo yaliyoletwa na Madini hayo kama vile barabara bora, shule, ujenzi wa vituo vya Afya na masuala mengine ya maendeleo.

“Sheria ya awali ilikuwa hainufaishi taifa na watanzania ndio maana mabadiliko yanafanyika.Mabadiliko ni kitu kizuri, tunahitaji rafiki atakayesababisha mabadiliko kutokea hivyo hawana haja ya kuogopa, tunawakaribisha kuwekeza alisisitiza Biteko.

(Visited 141 times, 1 visits today)
Share this post