ASSAs

KIFO CHA RUGE MUTAHABA: TUSIPOYASEMA HAYA, MAWE YATASEMA!!!

1616
0
Share:

Mamia ya waombolezaji wakimiminika kwenye mitandao ya kijamii kutoa salamu zao za pole kwa ndugu jamaa na marafiki wa Ruge Mutahaba, naye Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki Tundu Lissu kupitia ukurasa wake wa instagram ameandika waraka wake uliolenga kutoa salamu za pole.

Tundu Lissu, akiwa, Ubelgiji, ambapo anapatiwa matibabu ameandika” Ruge amefariki dunia nchini Afrika Kusini alikokuwa akitibiwa, ambapo alikuwa mmoja wapo wa wakurugenzi wa Clouds Media Group, moja wapo ya vyombo vya habari vikubwa hapa nchini Tanzania.

“Inaelekea huu ni msiba mkubwa sana kwa taifa letu. Viongozi wa Serikali, vyama vya siasa, taasisi mbali mbali na wananchi wa kawaida wamejitokeza hadharani kutoa salamu zao za rambi rambi kwa ndugu, jamaa na marafiki zake marehemu Ruge ” ameandika Lissu

Ameendelea “Naomba nikiri mapema: mimi sikumfahamu sana Ruge, nilikutana naye mara mbili au tatu aliponifuata Bungeni mwaka 2012 (kama sikosei) ili nisaidie kumpatanisha yeye na baadhi ya wanamuziki wa kizazi kipya, wakiongozwa na Mh. Joe Mbilinyi ‘Sugu, ‘ Nilifanya hivyo ” ameandika Lissu

Amesema kuwa, kutokana na kutomjua A to Z Ruge siwezi kumzungumza sana kwa mema au kwa mabaya yake kwa sababu siyafahamu sana, ila ninachotaka kukizungumzia ni haya maombolezo ya kifo chake.

Sikujua kwamba kumbe Ruge Mutahaba alikuwa “… kada wa CCM… aliyejijengea heshima na ukubalifu…” kwa Chama hicho, sikujua kwamba CCM ilimtumia Ruge sana wakati wa kampeni za uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, haya yote nimeyafahamu kufuatia kifo chake. Nimeyafahamu kwa sababu ya salamu za rambi rambi za Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole.

Mapema ya mwaka 2017, ofisi za Clouds Media Group zilizoko Mikocheni, Dar Es Salaam, zilivamiwa usiku na watu wenye silaha na sare za Jeshi la Polisi, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na wengine wakiwa wamevalia kiraia, watu hao waliongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam, Paul Makonda (Bashite) watu hawa walifanya uhalifu mbali mbali wa kijinai kwa mujibu wa sheria za nchi yetu.

Kwa bahati nzuri, tukio hilo lilirekodiwa kwenye kamera za video za ulinzi (CCTV), ambazo marehemu Ruge na wafanyakazi wa Clouds Media Group walizisambaza mitandaoni, kwa hiyo hadithi ya ‘watu wasiojulikana’ ilizoeleka haikuwezekana kwenye tukio hilo la kihalifu.

Kwa sababu ya kelele na shinikizo kubwa la umma, Waziri wa Habari, Michezo na Utamaduni wakati huo, Mh. Nape Nnauye, aliunda Kamati ya Uchunguzi wa tukio hilo, Jukwaa la Wahariri (TEF) na Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari (MOAT) nao waliunda Kamati za Uchunguzi.

Wachunguzi wote hawa walithibitisha pasina shaka yoyote kwamba Mkuu wa Mkoa Makonda aliongoza uhalifu huo,ambapo mara baada ya kupokea taarifa ya Kamati ya Uchunguzi aliyoiunda, Waziri Nape Nnauye alifukuzwa kazi na Rais John Magufuli.

Lissu amesema, Nape alipojaribu kufanya mkutano wa waandishi habari kuelezea tukio hilo, alizuiliwa kufanya hivyo kwa mtutu wa bastola ya maafisa wa Idara ya Usalama wa Taifa na Ujasusi (TISS), ambapo Jeshi la Polisi halikuchukua hatua yoyote ya kisheria dhidi ya Mkuu wa Mkoa Makonda na wavamizi wenzake wa Clouds Media Group.

Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), kupitia kwa Baraza lake la Uongozi, lilitoa kauli ya kulaani vikali uhalifu uliofanywa na Mkuu wa Mkoa Makonda na wavamizi wenzake. TLS iliazimia kufungua mashtaka ya jinai ya binafsi dhidi ya wahalifu hao, lakini hilo halikufanyika kufuatia kushambuliwa kwangu kwenye jaribio la mauaji la Septemba 7, 2017.

Rais Magufuli aliingilia kati na kuwa upande wa Mkuu wa Mkoa Makonda na wavamizi wenzake, Rais Magufuli alimfukuza kazi Waziri Nape Nnauye aliyejaribu kuingilia kati kwa niaba ya Clouds Media Group, Ruge Mutahaba na wafanyakazi wake.

Sasa Ruge Mutahaba amefariki dunia. Sasa hatasema tena. ‘Dead people tell no tales.’ Sasa ni salama kwa wabaya wake kujitokeza hadharani na kumlilia machozi ya mamba.

Ameongeza kuwa, sasa Chama alichokisaidia kupata madaraka halafu kikamkimbia wakati wa shida yake kinadai Ruge alikuwa na ‘ukubalifu’ ndani ya Chama hicho. Dead people tell no tales.

“Sasa ni wakati wa wanafiki kujitokeza hadharani, na wachawi kulia kwa uchungu kuliko waliofiwa, ni lazima tuyaseme haya sasa na hadharani,Tusipoyasema, hata mawe yatasema”ameandika Lissu

Mwenyezi Mungu ampe marehemu Ruge Mutahaba mapumziko ya amani. Na Mwenyezi Mungu atupe sisi tulio hai nguvu na ujasiri wa kusimama na kupaza sauti zetu kwa niaba ya akina Ruge waliopo na wale wajao.

(Visited 588 times, 1 visits today)
Share this post