ASSAs

MEYA WA UBUNGO AWAKUMBUKA WAKINA MAMA KWA KUWAPATIA MSAADA WA VIFAA VYA UJENZI

1825
0
Share:

Meya wa Ubungo, Boniface Jacob kwa kushirikiana na kampuni ya Speshoz wametoa msaada wa viwanda viwili vya ushonaji kwa vikundi viwili vya wanawake.

Viwanda hivyo viwili vya ushonaji kila kila moja kina seti ya vyerehani vitano ambavyo vimegharimu takribani Sh. Milioni 4.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wakikabidhi msaada huo, Meya Jacob amesema wamezindua programu hiyo ambayo itakuwa endelevu.

“Leo tunatoa msaada huu, na ndo tumezindua programu hii ambayo itakuwa endelevu ambayo lengo lake litakuwa kuwafikia kina mama wengi zaidi.

“Tumeshirikiana na Speshoz kusimamia kutoa msaada huu. Naomba ieleweke kuwa huu sio mkopo ni msaada, tumeona kutoa mkopo kila siku tutakuwa tunatumia vibaya msaada huu tuliopewa,” amesema Jacob.

Amesema vikundi hivyo viwili vyote vimetoka Manispaa ya Ubungo , na ni watu ambao walifika ofisi kwake kuomba kusaidiwa hivyo akawashauri wajisajili kama kikundi kisha kupatiwa msaada huo.

Naye Mkurugenzi wa Speshoz, Jefrey Jesse amesema mbali na msaada huo pia vikundi hivyo vitapatiwa mafunzo ya namna gani ya kuendesha biashara ya ushonaji.

Amesema watajitahidi kuhakikisha wanavisaidia vikundi hivyo viwanda vyao vinakuwa vikubwa.

“Unapompatia jembe mtu, lazima umfundishe na namna ya kulima, ndivyo ambavyo na sisi tutafanya kwa vikundi hivi. Ifike mahali nguo kama Jeans na nguo zingine ziwe zinatoka Tanzania na kwenda kuuzwa nje,” amesema Jesse.

Aidha ametoa wito kwa vikundi hivyo kutumia fursa hiyo kujiongezea vipato vyao pamoja na kuvikuza viwanda hivyo.

Mwenyekiti wa kikundi cha Victory Foundation, Betha Mwakasege ameshukuru kwa msaada huo, na kutoa wito kwa viongozi wengine kuiga mfano huo.

“Tunashukuru kwa fursa ambayo tumeipata. Meya Jacob ni kiongozi ambaye amekuwa akitusapoti sana, tunamhakikishia tutaitumia fursa hii vizuri na tunakwenda kukuza mitaji yetu,” amesema Betha.

(Visited 231 times, 1 visits today)
Share this post

Contact Us