ASSAs

TFF YATOA UFAFANUZI SHOMARI KAPOMBE KUJUMUISHWA KATIKA ZAWADI ILIYOTOLEWA NA RAIS MAGUFULI

1377
0
Share:

Uongozi wa Shirikisho la Soka nchini Tanzania TFF umetoa ufafanuzi  juu ya uwezekano wa mlinzi wa klabu ya Simba na Taifa Stars, Shomari Kapombe kujumuishwa katika zawadi iliyotolewa na Rais Magufuli kwa wachezaji wa Taifa Stars.

Katibu Mkuu wa TFF Wilfred Kidau, amesema kuwa suala la Kapombe kuhusika katika zawadi ya viwanja iliyotolewa na Rais Magufuli haliko mikononi mwao, bali lipo katika Ofisi ya Rais chini ya wasaidizi wake, amesema kuwa Ofisi ya Rais ndio wanafahamu ni wachezaji wangapi na namna gani ya kutoa zawadi hiyo, na kwamba wao TFF hawana mamlaka ya kuingilia mipango yao bali wanasubiri maelekezo.

Katika hatua nyingine Kapteni wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mbwana Ally Samatta, amesema yupo tayari kugawana nusu kwa nusu zawadi na beki Shomari Kapombe, endapo kama jitihada za kumpatia zawadi kama wachezaji wengine wa timu ya taifa zitashindikana.

Samatta ametoa ahadi hiyo leo, Machi 26, 2019 ikiwa ni siku moja imepita tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh John Magufuli alipotangaza kuwazawadia viwanja wachezaji walioiwezesha Taifa Stars kufuzu kwenye michuano ya AFCON 2019.

Katika ukurasa wake wa Twitter, Samatta ameandika kwamba “Kama Kaptein ningeomba TFF imuangalie Shomari Kapombe katika zawadi ambazo wachezaji watapata. Ikishindikana basi ningeomba wachezaji wote tumchangie kidogo kidogo”.

Ameongeza “Endapo vyote visipowezekana kabisa basi katika ahadi ya Mh Paul Makonda, nitagawana naye nusu kwa nusu”.

Ikumbukwe kuwa Shomari Kapombe alipata majeraha akiwa katika kambi ya Taifa Stars nchini Afrika ya Kusini, wakati wa maandalizi ya mchezo wa kuwania kufuzu michuano ya Mataifa y afrika AFCON dhidi ya Lesotho, mchezo ambao Taifa Stars ilipoteza kwa bao 1-0 ugenini mwezi Novemba mwaka 2018.

Jana Jumatatu, Machi 25, Rais Magufuli alikutana na wachezaji wa Taifa Stars, Kamati ya Uhamasishaji ya timu ya Taifa pamoja na Bondia Hassani Mwakinyo ikiwa ni siku moja baada ya timu hiyo kufuzu michuano ya Mataifa Afrika AFCON 2019, yatakayofanyika nchini Misri mwezi Juni hadi Julai.

 

(Visited 479 times, 1 visits today)
Share this post