ASSAs

AJIRA ZAIDI YA 4000 ZATANGAZWA NA SERIKALI

2406
0
Share:

Serikali kupitia Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(OR-TAMISEMI) imepata kibali cha kuajiri jumla ya walimu 4549  Kati ya 91108 walio tuma maombi yao.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo 27 April 2019 Magogoni, Dar es Salaam, Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI, Seleman Jaffo amesema kuwa Rais Dk.John Pombe Magufuli katika kuhakikisha Serikali inawahudumia vizuri wananchi ameamua kufungua dirisha la ajira kwa walimu.

Jaffo amesema jumla ya waombaji  91108 wamejitokeza na kutuma maombi yao katika nafasi mbalimbali na kati ya hayo 43770 sawa na asilimia  48.04  yalikuwa na viambatanisho vyote vilivyohitajika.

Hata hivyo alieleza kuwa maombi 47338 sawa na asilimia 51.96 hayakuwa na vigezo ikiwa ni pamoja na kukosa viambatanisho muhimu vilivyohitajika.

“Kutokana na mahitaji makubwa kwa walimu katika shule za msingi na sekondari  kwa masomo ya sayansi, Tamisemi imefanya uchambuzi  na kutoa  vipaumbele katika ajira  za walimu daraja la tatu (A) cheti kwa ajili ya kufundisha shule za msingi. Walimu daraja tatu (B) stashahada wa masomo ya sayansi kwa ajili ya kufundisha  shule za sekondari( kidato cha kwanza hadi nne); na walimu daraja la tatu (C)shahada, wa masomo ya sayansi kwa ajili ya kufundisha kwa kidato cha tano na sita,” amesema Jaffo.

Pia walimu daraja la tatu (C) shahada, wa masomo ya elimu maalum, biashara, uchumi, kilimo na maarifa ya nyumbani kwa ajili ya kufundisha shule ya sekondari.

“Mchakato wa kupitia maombi ulijumuisha uhakiki wa uhalali wa vyeti vya elimu ya taaluma vya waombaji na ukamilishaji wa nyaraka zilizohitajika,” amesema.

Aidha Jaffo ameeleza kuwa waombaji  wa masomo ya sayansi na sanaa waliotimiza vigezo  na hawakufanikiwa kupata nafasi kwa kipindi hiki, maombi yao yamechambuliwa na yamehifadhiwa kwenye kanzidata ya Tamisemi.

 Amesema kwa walimu hao pindi fursa za ajira zitakapojitokeza  utaratibu wa ajira utatolewa dhidi yao, “jumla ya walimu 4549 wamepangiwa moja kwa moja  kufundisha shule zilizo na uhitaji wa walimu ambapo 3059 shule ya msingi na 1490 kwa sekondari”.

Amewataka walimu wote waliopata ajira wanatakiwa kuripoti kwa wakurugenzi wa Halmashauri zenye shule walizopangiwa kwa ajili ya kuhakikisha vyeti vyao  na kujaza mikataba ya ajira kisha kuripoti kwenye vituo vyao kuanzia Mei 7, mwaka huu.

Jaffo alisema walimu wapya ambao hawataripoti katika vituo vyao ifikapo Mei 21, 2019 nafasi zao zitajazwa moja kwa moja na walimu walio na sifa ambao hawakupangiwa bila kuwataarifu.

“Wakurugenzi wa Halmashauri wasikubali kubadilisha vituo vya kazi vya walimu bila kibali cha Katibu Mkuu wa OR-TAMISEMI. Walimu hawa tumewapangia kulingana na mahitaji ya sehemu husika”.

Hatahivyo alisema kwa mwajiriwa atakayeripoti  na kuchukua posho ya kujikimu kisha akaondoka katika kituo chake cha kazi alichopangiwa atachukuliwa hatua kali za kisheria.

(Visited 1,020 times, 1 visits today)
Share this post