ASSAs

WAZIRI MKUU AWEKA WAZI BEI YA PAMBA KWA NCHI NZIMA

1144
0
Share:

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema ana imani kuwa ununuzi wa zao la pamba utaanza mara moja kwa bei ya sh. 1,200 kwa kilo moja katika mikoa yote inayozalisha zao hilo.

Amefikia uamuzi huo baada ya kuwepo kwa sintofahamu ya bei kwa takriban ya wiki nne tangu bei elekezi ilipotangazwa Aprili 30, 2019 mkoani Shinyanga kwamba bei hiyo ianze kutumika kuanzia Mei 2, 2019.

Alipokuwa akizungumza na wadau wa sekta ndogo ya pamba kwenye kikao kilichofanyika leo (Jumatano, Mei 29, 2019) kwenye ukumbi wa Chuo cha Benki Kuu, jijini Mwanza. Waziri Mkuu amewaeleza wajumbe wa mkutano huo kwamba Serikali bado inaendelea kutafuta njia nzuri ya kuwakutanisha wadau wa mazao ya kibiashara ili yaweze kuwa na tija kwa wakulima. 

Pia amesema Bodi ya Pamba iachiwe jukumu la kutoa leseni za ununuzi wa zao hilo na kwamba Wakurugenzi wa Halmashauri waliokuwa wakifanya kazi hiyo waache mara moja. “Kuna baadhi ya Wakurugenzi wanatoa leseni za ununuzi, lakini wenye Mamlaka ni Bodi ya Pamba. Mnunuzi nenda Bodi ukapate leseni yako,” amesema Waziri Mkuu.

Alitumia fursa hiyo kuwakemea baadhi ya wakurugenzi ambao wamekuwa wakizuia wanunuzi wapya kwenye maeneo na kuendelea kuwakumbatia wanaowataka wao. “Wakurugenzi baadhi yenu mnazuia wanunuzi wapya, mnamtaka fulani tu. Kwa kufanya hivyo, unapungua kiwango cha kilo ambacho wakulima wako wangeuza,” alionya.

Kuhusu ubora wa pamba, Waziri Mkuu ametaka wananchi waelimishwe ili waache kuweka maji au mchanga kwenye pamba kwa minajili ya kuongeza uzito kwani kwa kufanya hivyo wanachafua jina la Tanzania pindi inapopelekwa kuuzwa nje ya nchi.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mhandisi Mathew Mtigumwe atume wakaguzi kwenye Bodi ya Pamba ili wabainishe matumizi ya sh.100 kwa kila kilo ambazo zimekuwa zikilipwa kwenye bodi hiyo.

“Na Mrajisi wa Ushirika nchini ufanye ukaguzi kwenye vyama vikuu vya Ushirika na AMCOS. Uangalie ziko ngapi na zinafanya nini. Kuna AMCOS zina hela, je fedha hiyo imetumika kufanya nini ili kuendeleza zao la pamba. Je zimenunua matrekta au zimelipia posho za vikao,” amesema.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wanunuzi Binafsi wa Pamba (TCA), Bw. Christopher Gachuma ameshukuru Waziri Mkuu kwa maelekezo aliyoyatoa kuhusu utoaji wa leseni kwani yalikuwa ni kikwazo kikubwa kwa baadhi ya wanunuzi wa zao hilo.

(Visited 78 times, 1 visits today)
Share this post