ASSAs

WAZIRI UMMY ATOA MIEZI 3 KUKAMILISHA MRADI WA UJENZI WA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA GEITA

579
0
Share:

Na WAMJW- GEITA

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amefanya ziara katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kukagua miradi ya ujenzi wa Hospitali za Rufaa za mikoa nchini.

Katika ziara hiyo Waziri Ummy amemwagiza Mkandarasi kutoka TBA Mkoa wa Geita kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha ndani ya miezi mitatu mradi huo unaisha ili huduma za Afya zianze kutolewa ifikapo Disemba 1, 2019.

“Nimemtaka Mkandarasi afanye kazi usiku na mchana ikiwezekana tukamilishe ujenzi huu hata mwezi wa kumi mwishoni, lengo langu nataka tarehe 1 mwezi Disemba 2019, tunaanza kutoa huduma hapa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita” alisema Waziri Ummy.

Aidha, Waziri Ummy amesema kuwa Serikali imetoa kiasi cha shilingi Bilion 2.5 ili kukamilisha awamu ya kwanza ya ujenzi wa Hospitali hiyo, ambayo itajenga jengo la wagonjwa wa nje (OPD), jengo la Maabara, jengo la upasuaji pamoja na jengo la mionzi.

Hata hivyo, Waziri Ummy amesema kuwa licha ya kuwepo changamoto ya upungufu wa Watumishi katika Sekta ya Afya, Wizara ya Afya imepata kibali cha kuajiri Watumishi wengine kutoka Wizara ya Utumishi jambo litalosaidia kupunguza Uhaba wa Watumishi katika Sekta ya Afya.

Waziri Ummy aliendelea, kwa kuwataka Wakurugenzi kujiongeza ili kupambana na uhaba wa Watumishi katika ngazi ya Mkoa, ikiwemo kuajiri baadhi ya Watumishi kupitia mapato ya ndani ili kupunguza changamoto ya uhaba wa Watumishi, huku akitoa Wito kwa vijana waliomaliza vyuo kujitolea katika Hospitali ili kuongeza uzoefu zaidi.

Mbali na hayo, Waziri Ummy amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli kwa kuendelea kujali Afya za Watanzania kwa kuboresha Sekta ya Afya ikiwemo kuboresha miundombinu ya Hospitali na kuhakikisha Dawa, vifaa na vifaa tiba vinapatikana.

Nae, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel amemuomba Waziri Ummy kuanza kwa awamu ya pili ya ujenzi wa Hospitali hiyo ili kupata wodi ambazo zitatumika kulaza wagonjwa wataofika kupata huduma za Afya

“Uwepo wa wodi ndio utatoa taswira ya kuwa Hospitali hii kuwa ni Hospitali ya Mkoa, ili mtu akipata Rufaa aweze kulazwa na kuchukuliwa vipimo” alisema Mkuu wa Mkoa Mhandisi Robert Gabriel

(Visited 49 times, 1 visits today)
Share this post