ASSAs

TEWW IMEJIPANGA KUWAFIKIA VIJANA WALIOKOSA ELIMU

1150
0
Share:

Taasisi ya elimu ya watu wazima (TEWW) imesema imejipanga kuwafikia vijana wengi zaidi walionje ya shule na wale walioenda shule lakini hawajui kusoma na kuandika, lengo ikiwa ni kuwafanya wajitambue na kuona wanathamani ya kuendelea kuishi.

Kauli hiyo imetolewa Jijini Dar es Salaam na Mkuu wa idara ya elimu kwa umma shule huria, Placid Balige wakati alikuwa akizungumza na waandishi habari kwenye maonesho ya 14 ya Vyuo vya elimu ya juu sayansi na Teknolojia yanayofanyika katika viwanja vya mnazi mmoja.

Amesema kuwa, ili kuhakikisha wanawafikia vijana wengi zaidi wameandaa mradi mpango wa elimu changamano (IPOSA) ambayo itawawezesha vijana hao kuweza kujitambua kusoma, kuandika na pamoja stadi za maisha ikiwemo kujifunza ujasiriamali.

“Licha ya kuwepo kwa elimu bure lakini tunawaona vijana bado wapo mtaani hii ina maana kwamba wanamatatizo zaidi ya hayo, hivyo ndio maana tumewekeza zaidi katika kuwafundisha stadi za maisha ili waweze kumudu maisha yao”amesema Balige.

Ameongeza kuwa, kwa upande wa watoto waliopata ndoa za mapema na kukatisha masomo yao wamepata mafanikio makubwa kwani wamewafundisha stadi za maisha ikiwemo kuweza kujiajiri wenyewe hali iliyopelekea baadhi yao kuweza kujilipia kurudi shule.

Amesema kuwa, watoto hao wameweza kufungua maduka na kuweza kuzalisha bidhaa zao wenyewe ikiwemo kutengeneza sabuni, kusindika chakula pamoja na kupata mkopo wa asilimia 4 wa vijana unaotolewa na manispaa kwa lengo la kuwakomboa vijana.

“Tumeweza kuwafikia vijana 3000 katika mkoa wa Dodoma,Rukwa na Lindi ambao walipata ndoa za mapema na kukatisha masomo yao kwa sasa wameweza hata kujiunga Vikundi na kuweza kupata mkopo wa Manispaa wa asilimia 10 unatolewa nchi nzima ” amesema Balige.

Aidha amesema, taasisi hiyo inatoa elimu kwa ngazi ya elimu ya juu, stashahada pamoja na astashahada ambapo asilimia kubwa ya wanafunzi wao ni wafanyakazi hivyo ujuzi huo huwafikia walengwa moja kwa moja katika ngazi ya wilaya na kata ambapo kampasi zao zipo Dar es Salaam, Morogoro-WAMO na Mwanza-Luchelele.

(Visited 300 times, 1 visits today)
Share this post