ASSAs

KAMATI YA KITAIFA YA URATIBU NA UTHIBITI WA USUGU WA VIMELEA DHIDI YA DAWA YAZINDUA WIKI YA UHAMASISHAJI MATUMIZI YA ANTIBIOTIKI NCHINI

693
0
Share:

KAMATI YA KITAIFA YA URATIBU NA UTHIBITI WA USUGU WA VIMELEA DHIDI YA DAWA YAZINDUA WIKI YA UHAMASISHAJI MATUMIZI SAHIHI YA ANTIBIOTIKI NCHINI

NA ANDREW CHALE

KAIMU Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Eliasi Kwesi amezindua rasmi shughuli za kuhamasisha matumizi sahihi ya dawa za Antibiotiki katika kuelekia wiki hiyo duniani itakayofanyika kuanzia Novemba 18-24, mwaka huu duniani kote.

Katika tukio hilo, Dkt. Kwesi alimwakilisha Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu ambapo alitaka jamii kuelewa athari na tatizo kubwa ambalo limekuwa likiongezeka duniani kote litokanalo na usugu wa vimelea dhidi ya dawa.

“Kuanzia tarehe 18-24 Novemba, mwaka huu, duniani kote tunaadhimisha wiki ya kampeni ya dawa aina ya Antibiotiki (World Antibiotic Awareness Week).
Lengo ni kusisitiza na kuongeza uelewa juu ya matumizi sahihi ya dawa hizi ili kupunguza matumizi yasiyostahili na hatimaye kuzuia ongezeko la usugu wa vimelea dhidi ya dawa hizi” alieleza Dkt. Kwesi.

Aidha, alisema kuwa, Serikali imendaa mipango na miongozo mbalimbali ili kutekeleza kazi kwa usahihi ikiwemo mpango wa Taifa wa kupambana na usugu wa dawa dhidi ya vimelea mbalimbali Antimicrobial ( 2017-2022).

“Niwaagize watoa dawa kote nchini kuandika dawa kwa kufuata mwongozo wa matibabu wa mwaka 2017 na kutumia majina halisi ya dawa (Generics).

Pia naagiza vituo vyote vya huduma ya afya kutekeleza miongozo ya kukinga na kuzuia maambukizi ambayo ni muhimu sana kwa kuzuia usugu katika sehemu zao za kazi” alisema Dkt. Kwesi.

Aidha, akielezea ripoti ya benki ya Dunia ya mwaka 2017 inabainisha kuwa zaidi ya watu 700,000 wanafariki kila mwaka kutokana na usugu wa dawa.

“Hatua madhubuti zisipochukuliwa haraka zaidi ya watu milioni 10 watafariki kila mwaka kutokana na usugu wa dawa ifikapo mwaka 2050.

Hali hii ya usugu wa vimelea inaweka mashaka makubwa ya kupoteza nguvu kazi ya Taifa hili kwa kusababisha vifo kutokana na kuongezeka kwa magonjwa sugu yasiyotibika kwa kutumia dawa zilizokuwa na uwezo wa kutibu, kuongezeka kwa umasikini kutokana na kuugua muda mrefu na kutumia dawa ghari zaidi lakini pia kuongezeka kwa vifo vya mifugo na udhalishaji hafifu wa chakula” alieleza Dkt. Kwesi.

Dkt. Kwesi alitoa wito kwa jamii kuzingatia matumizi sahihi ya kuepukana hasa kwenye kinga ya maambukizi kwa njia ambazo zinaweza kufanywa mahali popote ikiwemo ngono salama, kuosha mikono na chanjo.

Hata hivyo Dkt. Kwesi alizitaka Wizara zingine wadau wakiwemo Mawaziri wa Mifugo na uvuvi,, Kilimo na Mazingira kwa pamoja kufanya kampeni zinazolenga kuongeza uelewa wa jamii juu ya matumizi sahihi na athari zitokanazo na matumizi holela ya dawa kwa binadamu na mifugo.

Kwa upande wao wadau walioshiriki katika tukio hilo wakiwemo wawakilishi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa, Shirika la Afya (WHO), Shirika la Chakula (FAO) na Shirika la Wanyama (OIE) walieleza wanashirikiana kwa pamoja na Serikali ya Tanzania katika mapambano ya tatizo hilo.

Mwisho.

(Visited 95 times, 1 visits today)
Share this post

Contact Us