ASSAs

MAKAMU WA RAIS SAMIA SULUHU KUWA MGENI RASMI MAFUNZO YA UJASIRIAMALI YA WANAWAKE (BAKATWA)

305
0
Share:

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), kwa ajili ya kuzindua mafunzo ya kuwawezesha wanawake wa Kiislamu kiuchumi.

Katika mafunzo hayo inatarajiwa wnawake zaidi ya 3,000 wa kiislamu  watapata mafunzo hayo kwa lengo kuwawezesha  kufikia uchumi wa viwanda.

Akizungumzia leo Januari 14, 2020, Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam Alhadi Mussa Salum amesema mafunzo hayo yatafanyika Januari 25, mwaka huu kuanzia saa tatu asubuhi ambayo itakuwa bure.

“Kama tunavyojua Serikali ya Awamu ya Tano imekuja na sera ya Tanzania ya viwanda, na Bakwata imeona ipo haja kufanya warsha hii maalum katika kuwafikia wanawake ambao wengi wao hawana uelewa mpana kuhusu masuala ya viwanda na  hata taasisi zinazoshughulikia mambo ya viwanda nchini,”amesema.

Ameongeza wanawake wengi kupitia mafunzo hayo watapata elimu sahihi na kutambua fursa zilizopo nchini kwa kujishughulisha na shughuli mbalimbali za ujasiliamali au kufanya kazi.

Sheihk Alhad ameongeza kufanya kazi ni ibada kwa mwanamke na mwanaume kwani hata dini imeelekeza mwanaume na mwanamke wote wanahaki sawa ya kumiliki mali.

“Ili uweze kumiliki mali ni lazima ujishughulishe, ufanye kazi, biashara hili katika Uislamu ni tofauti na watu wanavyoliangalia kwamba mwanamke wa kiislamu ni wa kukaa tu.

“Anaweza akakaa lakini akiamua kujishughulisha anajishughulisha kwa masharti yanayotakiwa kwa mujibu wa dini na mipaka ya dini yake,”amesema.

Amesisitiza wanawake wa Kiislamu ni kama wanawake wengine ambapo zipo fursa wanatakiwa wazitumie ili nao watoe mchango wao kwa Serikali kuhusu uchumi wa viwanda.

Ameongeza kufanyika kwa mafunzo hayo kutachangia kufungua fursa za kiuchumi hasa kwa wanawake wenye uelewa mdogo.

“Mada mbalimbali zitatolewa siku hiyo, wadau wa uchumi na viwanda watatoa mada mbalimbali, kila mmoja atawasilisha mada siku hiyo Tanzania wa viwanda inawezekana kwa kumjali mwanamke,”amesema.

(Visited 28 times, 1 visits today)
Share this post