ASSAs

SERIKALI YATOA NENO KUHUSU USAJILI MPYA WA WANAHABARI

364
0
Share:

SERIKALI imewataka waandishi wa habari nchini kujiendeleza kitaaluma ili kukidhi vigezo vya Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016, inayowataka ifikapo 2021 kuwa na elimu ya stashahada (diploma).

Akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka ujao wa fedha, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, alisema sheria ilitoa kipindi cha miaka mitano kwa kila mwanahabari kuwa na kiwango hicho cha elimu na kitafika kikomo mwakani.

“Kwa kuwa kipindi hiki cha miaka mitano kinakwisha mwezi Desemba 2021, natoa wito kwa waandishi wa habari ambao bado hawajajiendeleza kielimu, ili kukidhi matakwa ya sheria wafanye, hivyo ili kuendelea na kazi ya uandishi wa habari baada ya muda huu wa mpito kuisha,” alisema.

Waziri Mwakyembe alisema Wizara ipo katika hatua za mwisho za uanzishwaji wa Bodi ya Ithibati ya Wanahabari, ikiwamo Baraza Huru la Habari ambalo litaundwa na wanahabari wenyewe baada ya kuanzishwa kwa bodi hiyo.

“Majukumu ya Baraza hili ni pamoja na kuandaa Kanuni za Maadili ya Taaluma ya Wanahabari kwa kushirikiana na Bodi ya Ithibati na kushughulikia malalamiko mbalimbali ya maudhui chini ya Kamati ya Malalamiko iliyoundwa ndani ya baraza,” alisema.

Alisema hadi kufikia Machi mwaka huu, magazeti na majarida 233 yalisajiliwa ili kupanua wigo wa upatikanaji wa habari kwa wananchi, na kwamba kati yake binafsi ni 181 sawa na asilimia 78 na serikali na taasisi zake 52, sawa na asilimia 22.

Alisema leseni mpya 18 zilitolewa kwa ajili ya magazeti/majarida ambapo 14 zilitolewa kwa wamiliki binafsi na nne kwa taasisi za umma, na kwamba leseni 43 zilihuishwa, ikiwamo kutoa vitambulisho kwa wanahabari 494. Kati yao, saba ni wa nje ya nchi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Peter Serukamba, alisema kuwa hadi kufikia Februari mwaka huu, wizara ilikuwa haijafikia hata nusu ya lengo la makusanyo kwa kuwa ilikuwa imekusanya Sh. bilioni 14.5, sawa na asilimia 37.7 ya lengo.

Naibu Waziri Kivuli katika wizara hiyo na Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Devotha Minja, aliitaka Wizara ya Afya kutoa taarifa za corona kila baada ya saa kadhaa ili kuendeleza tahadhari.

“Nikiangalia taarifa ya habari, naona waandishi wa nchi nyingine wanavyoripoti kuhusu corona kila siku, tunaona mawaziri wao wakitoa takwimu, ila hapa kwetu ni baada ya siku kadhaa ndiyo zinatolewa, hii siyo sawa tunahitaji taarifa kila mara,” alisema.

Pia, alitaka waandishi wa habari kulindwa katika utekelezaji wa majukumu yao kwa kuwa wengi hawana vifaa vya kisasa na kuwasogelea wanaohojiwa kiasi cha kuwa katika hatari kubwa ya kupata maambukizo.

(Visited 34 times, 1 visits today)
Share this post

Contact Us