ASSAs

DK. HUSSEIN MWINYI NA NJIA ALIYOIPITA JPM

434
0
Share:

Wakati wa mchakato wa kuwania kupitishwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa mgombea Urais kwa mwaka 2015, wagombea 38 walijitokeza kutaka kuwania nafasi hiyo huku kila mmoja akieleza ni kipi atawafanyia Watanzania akipewa nafasi.

Mgombea mmoja hakutaka kuahidi chochote bali yeye alisema atatekeleza kile ambacho CCM itakuwa imekipitisha kwenye Ilani ya Uchaguzi ya 2015-2020. Mgombea huyo hakuwa mwingine bali Dk. John Magufuli – Rais wa sasa wa Tanzania.

Dk. Magufuli hakuwa mgombea wa kawaida. Pamoja na kuwa kwake katika Baraza la Mawaziri kwa marais wawili; Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete – hakukuwa na mtu aliyekuwa akifahamu hasa msimamo wake kuhusu mambo mengi yaliyotokea nchini.

Hakuna mtu aliyewahi kuwa amemsikia Magufuli akizungumza kuhusu Jumuiya ya Afrika Mashariki, uhusiano wetu na nchi za kigeni, kuhusu kashfa kama Richmond, Escrow na mambo mengine.

Magufuli alikuwa akisikika kwenye kazi zake za ujenzi wa barabara, kwenye mambo ya uvuvi alipokuwa waziri wa wizara hiyo na hakuwa akitoa maoni yake nje ya eneo lake.

Kwa sababu hiyo, Magufuli akawa mgombea ambaye watu hawakujua mengi sana kumhusu yeye, lakini ndiye akaja kuwa kinara miongoni mwa wenzake.

Japokuwa alishakuwa waziri kwa takribani miaka 20, wengi wa wabunge wenzake walielezea kutomjua kwa kiwango kikubwa kiasi cha kutojua hata vitu anavyovipenda nje ya siasa.

Hadithi hiyo inafanana na ya Dk. Hussein Mwinyi anayewania nafasi ya kutaka kupitishwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwania urais wa Zanzibar.

Siku aliyokwenda kuchukua fomu ya kuwania urais katika Ofisi za Chama Kisiwandui, waandishi wa habari walitaka kumbana kwa maswali awaeleze mipango yake lakini yeye alijibu –kiungwana, kwamba apewe kwanza nafasi asome makabrasha aliyopewa na chama kabla ya kusema chochote.

Na baada ya kurejesha fomu wiki iliyopita, Dk. Mwinyi pia hakutaka kusema lolote. Ni tofauti na mgombea kama Balozi Ali Karume, ambaye alitumia fursa hiyo kueleza mipango yake yote.

Hussein Mwinyi ni mmoja wa mawaziri wazoefu katika Baraza la Mawaziri la Rais John Magufuli. Ukimuondoa Rais, ni yeye na Waziri wa Ardhi, William Lukuvi, ndiyo ambao wamekuwa mawaziri tangu wakati wa utawala wa Rais Benjamin Mkapa.

Katika muda wote huo, hakujawahi kuwa na kashfa wala tukio la kumwaibisha kisiasa lililowahi kutokea chini yake. Na tangu aingie katika baraza hilo, hajawahi kutoka.

Yeye, Magufuli na Lukuvi wamekuwa tu wakihamishwa kutoka wizara moja kwenda nyingine katika nyakati tofauti lakini bado wameendelea kubaki mawaziri kwa muda wote hadi Magufuli alipopanda zaidi na kuwa Rais.

Katika wakati wake akiwa ndani ya Bunge na serikalini, mambo mengi yametokea lakini anayejua yeye alikuwa na mtazamo au msimamo upi kuhusu hayo?

Mwinyi hajawahi kuzungumza hadharani kuhusu mambo mengi mazito yaliyowahi kutokea hapa nchini. Hatukumsikia wakati wa kashfa ya Richmond, kwenye Escrow wala mambo ya Lugumi.

Kwa wadhifa wake kama Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), ni wazi kwamba Dk. Mwinyi ana taarifa za kutosha kuhusu nini kinachoendelea hapa nchini. Hata hivyo, mara zote ameamua kubaki kimya na kubaki na mawazo yake sirini mwake.

Endapo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitaamua kumpitisha Dk. Mwinyi kuwa mgombea wake, ujumbe utakaokuwa umetolewa na chama ni kuwa sasa kimeamua kuangalia utendaji wa mtu na changamoto zilizopo wakati husika badala ya umahiri wa kuzungumza bungeni au majukwaani.

Utaratibu huu ndiyo ambao sasa umepewa jina jipya la “New Normal” katika maeneo mbalimbali duniani. Kwamba dunia inaachana na zama za kuchagua viongozi wanaojulikana sana kwa maneno na kuchukua wengine wasiofahamika kwa umahiri wa kuzungumza jukwaani au kupiga maneno.

Uhuru Kenyatta alipata Urais wa Kenya bila kujulikana sana kwa watu – ukiachia jina la baba yake. Hakuna aliyesema anamfahamu Uhuru kwa sababu aliwahi kutoa msimamo kuhusu jambo fulani au kuibua kashfa bungeni.

Macky Sall wa Senegal naye alichaguliwa na chama chake na wananchi wake pasipo kujulikana kwa kuzungumza sana au kutoa maoni kuhusu masuala tofauti. Vyombo vya habari vya Senegal viliamua tu kusema kwamba havitegemei mhandisi kuwa na maneno mengi wakati alipoibuka kwa mara ya kwanza mwaka 2007.

Kwa upande mwingine, kuna Waziri Mkuu Abiy Ahmed wa Ethiopia ambaye alipewa nafasi na chama chake kutokana na namna wanavyomjua kwa uchapaji kazi wake na mapenzi kwa taifa lake. Huyu naye ni mwanasayansi, akitengeneza jina lake kama mtaalamu wa masuala ya mifumo ya mawasiliano ya kompyuta.

Kwa hiyo, Rais Magufuli mwaka 2015 na Dk. Hussein Mwinyi wa mwaka 2020, wanawakilisha kizazi kipya cha wanasiasa wa Afrika ambao wamebadili mtazamo kutoka watu wenye maneno mengi na kuleta watu wanaoyajua matatizo ya nchi zao na suluhisho lake.

Kizazi hiki cha viongozi wapya wa Afrika kimeanza kujipambanua kwa kuthamini zaidi kazi na maendeleo badala kuzungumza mambo yanayowafurahisha watu wa ndani na nje ya nchi.

Senegal ya Sall sasa imejipatia umaarufu kutokana na jitihada zake za kupambana na ugonjwa wa Korona kwa wataalamu wake kubuni vifaa vya kupimia watu vilivyo nafuu kuliko vile vya nchi zilizoendelea.

Abiy naye ametumia fursa ya ugonjwa wa Korona kulifanya Shirika la Ndege la Ethiopia kuwa msafirishaji mkuu wa vifaa tiba barani Afrika; likifanya kazi wakati mashirika mengi yakiwa yamefunga shughuli zake.

Rais Magufuli yeye amejipatia sifa kwa kushughulika na ugonjwa huo wa Korona kwa namna ambayo hakuna kiongozi mwingine wa dunia amefanya. Njia zake za kukabiliana na mambo haziigi uzoefu kutoka nchi nyingine bali zinazingatia uelewa wake wa watu wake na linaloweza kufanyika.

Kama ilivyo kwa Sall, Abiy na Magufuli, Mwinyi naye pia ni mwanasayansi. Sall ni mhandisi, Magufuli ni mkemia na mgombea huyu wa Urais wa Zanzibar kupitia CCM yeye ni daktari.

China walibaini mapema sana umuhimu wa viongozi waliosomea masomo ya sayansi wakati wakijitahidi kutoka kuwa nchi masikini kwenda kuwa nchi tajiri.

Kuna wakati, zaidi ya nusu ya wajumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti walikuwa ni watu waliosomea masomo ya kisayansi wakiaminika kuwa wangefaa kuitengeneza China ya viwanda.

Rais wa China, Xi Jinping, ambaye naye si mzungumzaji sana lakini ni mtendaji wa kiwango cha juu na sasa akiwa anarejesha heshima ya taifa hilo duniani, naye alisomea masomo ya uhandisi wakati akisoma Chuo Kikuu nchini kwao.

Huenda tabia hii ya Hussein Mwinyi kuwa mkimya au kutopenda kujiingiza katika mambo yasiyomhusu ni ya kawaida kwa wanasiasa waliosomea masomo ya sayansi.

Na kama Watanzania walijifunza kitu kupitia uchaguzi wa mwaka 2015, basi jambo hilo ni kwamba muhimu ni kwa chama kujua kinataka mgombea wa namna na wakati gani.

Kutopiga mdomo vya kutosha si sababu ya kushinda au kushindwa kwenye mchakato wa chama au dhidi ya vyama vingine.

Hili tayari Rais Magufuli ameshalizungumza. Na inaonekana Mwinyi amejifunza na anapita katika njia zilezile alizopita bosi wake.

(Visited 208 times, 1 visits today)
Share this post